Walisema penzi letu
mwishowe litopunguka.
Walisema jua letu litazama
na giza itatanda.
Walisema rohoni utanitoka.
Walisema penzi letu litafifia,
libaki mazoea.
Waongo hao.
Waongo hawajapata
kuvutiwa na penzi.
Waongo hawajapata
kuridhishwa na penzi.
Waongo hawajui
macho yaliona wengi
lakini yakakuchagua wewe;
Kwa hao hakuna niliyemuenzi.
Waongo hawajui
moyo wangu ulipoa
kizuri nilipokipata.
Waongo hawajiulizi
“mbona kanipenda wewe
na penzi ukanitwika?”
Waongo hawajatambua
sitochoka na sitokuacha;
hatokuja mwengine.
Waongo hawajajua
tusharidhiana wenyewe
na hatuwaombi chao;
Waongo hawajakubali
tumependana wenyewe,
waamini wasiamini.
Waongo hawajui
ahadi tulizotoa
zilitimia pale
dunia iliposhuhudia,
na Mungu akapenda
na akatia sahihi.